Nav bar

Ijumaa, 3 Novemba 2017

WAFUGAJI TEMBEENI KIFUA MBELE WAZIRI MNAYEE- MPINA

NA: MWANDISHI MAALUM - KATERERO KAGERA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina  amewataka wafugaji nchini kutembea kifua mbele kwa kumpata yeye kama Waziri mwenye dhamana ya Mifugo, Mpina ameyasema hayo jana aliposhiriki katika zoezi la kupiga chapa Mifugo  katika Kijiji cha Kyelwa kilichopo katika kata ya Katerero Halmashauri ya Wilaya Bukoba mkoani Kagera,  na kuwataka viongozi kuzingatia maadili wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo ili kuepuka hujuma na ubaguzi kwa wafugaji.

Waziri Mpina alipofika katika kata ya  Katerero aliwakuta wafugaji wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono zoezi la upigaji chapa katika mifugo yao na kushiriki zoezi hilo kwa kuonyesha msisitizo.

Waziri Mpina aliwataka wafugaji  kuleta mifugo yao kupigwa chapa na kusisitiza kwamba zoezi hilo ni la manufaa na faida kwa wafugaji kwani litaweza kuwasiadia kuepuka maambukizi ya magonjwa ya wanyama kwa mifugo yao kwa kutokuchanganyikana na mifugo mingine sambamba na kusaidia upotevu wa mifugo.

Akiongea katika zoezi hilo diwani wa kata ya Katerero Bw. Nuru Abdul Kabendera alisema kuwa, amefurahishwa na ziara ya Waziri Mpina katika kata ya katerero kwani ni mara ya kwanza kwa kata hiyo kupata ugeni kutoka katika ngazi ya juu ya serikali na kumuomba Mpina kupitia Wizara yake kutatua changamoto inayoikabili kata hiyo la  josho la kuoshea ng’ombe ambapo Waziri Mpina amehaidi kuitatua.

Katika hatua nyingine Waziri Mpina ametembelea mapori ya Burigi yaliyopo wilayani Biharamulo ambapo ameupongeza uongozi wa mkoa kwa uperasheni iliyofanyika ya kuondoa mifugo katika mapori tengefu na hifadhi za misitu ambapo amewashuhudia wanyama pori ambao tayari wamerejea katika mapori hayo huku mkuu wa wilaya hiyo Bi Saada Malunda akiwataka wananchi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano katika zoezi la kuondoa mifugo.

Aidha, Mpina amewataka wakuu wa Mikoa ya mipakani kuwasilisha kwake taarifa ya uondoshwaji wa mifugo katika mikoa yao mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la oparesheni ondoa mifugo.

Waziri Mpina amemaliza ziara yake ya siku mbili mkoani kagera kubwa akiwa ameagiza mifugo yote iliyokamatwa kutoka nje ya nchi itaifishwe na kupigwa mnada haraka sana kwa mujibu wa sheria.



Waziri Mpina na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Bukoba wakielekea katika zoezi la upigaji chapa ng'ombe katika kata ya katerero kijijini Kyelwa jana.

Katika picha inaonekana sehemu ya ng'ombe aliyepigwa chapa katika kata ya katerero kijijini Kyelwa jana

Picha ya pamoja ikimuonyesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina, Mkuu wa Wialaya ya Biharamulo Bi, Saada Malunde baada ya zoezi la kukagua uvamizi wa mifugo katika sehemu ya pori la Bugiri Biharamuro, wengine katika picha ni askari wanyamapori wa pori hilo.

Mpina akiongea na wanahabari mara baada ya ukaguzi wakati wa oparesheni ondoa mifugo katika sehemu ya pori la Bugiri Biharamulo, Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bi Saada Malunde.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni