WANUFAIKA WA PROGRAMU YA UWEZESHAJI VIJANA KIUCHUMI SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI WAPATIWA MAFUNZO DODOMA
Na. Martha Mbena.
Wanufaika wa Uwezeshaji wa Programu ya Vijana kiuchumi katika Sekta za Mifugo na Uvuvi wapatao 45 kwa mkoa wa Dodoma wamepatiwa mafunzo kwa lengo la kusimamia miradi yao kwa ufanisi, kutumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuongeza ajira pamoja na uzalishaji katika sekta hizo.
Mafunzo hayo yametolewa Julai 30.2026 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo wanufaika hao wamepata ujuzi wa namna bora ya ufugaji wa Nguruwe, Ufugaji wa kuku, Ufugaji wa Kondoo, utengenezaji wa Malisho ya Mifugo na mambo Muhimu ya kuzingatia kabla ya kuanza uwekezaji.
Daktari wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Pius Bunga. Ambaye pia ni muwezeshaji wa mafunzo hayo, Amewapongeza wanufaika wa mikopo hiyo na kuwasisitiza kuzingatia malengo ya kuanzishwa kwa programu za ufugaji na kuweka nidhamu ya katika usimamizi wa fedha watakazokopeshwa ili kuweza kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa Nchi.
“Hii fursa ambayo mnaipata nawasihi muifanye kwa moyo ili kuweza kufanya vizuri na kuweza kurejesha mkopo ambayo mtakwenda kupata hivi karibuni”. Amesema Dkt. Bunga.
Aidha, mafunzo hayo yamesisitiza umuhimu wa kufuatilia matumizi ya mikopo, kukusanya na kuhifadhi taarifa za utekelezaji wa miradi, kutambua changamoto zinazoweza kujitokeza na kuhakikisha sheria, kanuni na viwango vya kitaalamu vinafuatwa wakati wote wa utekelezaji.
Kwa upande wake Mfugaji wa kuku wa mayai ambaye pia ni mnufaika wa mkopo huo Bw. Elia Lukiko kutoka Halmashauri ya Dodoma, ameishukuru serikali na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa mafunzo hayo kwa Wafugaji kwani itawasaidia kufuga kisasa na kupata faida na kuongeza kipato cha Mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Vilevile, wanufaika wamekumbushwa wajibu wa kutafuta masoko ya bidhaa zao, kutunza kumbukumbu za uzalishaji, kutoa taarifa za maendeleo ya miradi kwa mamlaka husika, na kurejesha mikopo kwa wakati kulingana na makubaliano na benki.
Mafunzo hayo pia yameeleza kuwa wanufaika wanawajibika kutunza mali za mradi, kulipa kodi na tozo zinazotakiwa kisheria, huku wakihimizwa kushirikiana na wasimamizi wa programu katika ufuatiliaji na tathmini ya maendeleo ya miradi.
Kupitia mafunzo hayo, Serikali inatarajia kuwa vijana watanufaika zaidi na fursa za mikopo, wataendesha miradi yenye tija na kuchangia ukuaji wa sekta za mifugo na uvuvi pamoja na maendeleo ya uchumi wa taifa.






Maoni
Chapisha Maoni