Kurasa

Jumatano, 24 Desemba 2025

"SITACHOKA KUWASEMEA, KUWAPAMBANIA VIJANA WA KITANZANIA" - MHE. NG'WASI

 Na, Hamisi Hussein, Singida 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi  ambae pia ni Mbunge wa Kundi la Vijana kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Ng'wasi  Damas Kamani, amesema  ataendelea kulisemea, kulitetea na kulipambania kundi la vijana kupata fursa mbalimbali za kujiinua kiuchumi hususani katika sekta ya mifugo na uvuvi.

Mhe. Ng'wasi  ameyasema hayo leo Desemba, 24, 2025, Wilayani Iramba Mkoani Singida, alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika Kikao cha Baraza la Kawaida la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo.

  "Pamoja na majukumu haya niliyopewa sitachoka kumtetea, kumsemea na kumpambania kijana wa kitanzania, lakini pia hata katika sekta hii ninayoisimamia huku ndio nitaweka nguvu zaidi ili ikiwezekana na sekta zingine ziige  kutoka kwetu namna ya kumsaidia kijana wa kitanzania"amesema N'gwasi.

Katika hatua nyingine Mhe. Ng'wasi amesema yuko tayari kushirikiana na vijana katika kuzifikia fursa za kiuchumi na kuwahimiza vijana hususani wa Chama cha Mapinduzi kuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani nchini pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Mhe. Rais Samia ametuamini vijana na ametupa nafasi ili masuala yanayohusu vijana tuyaamue wenyewe, ni jukumu letu kumuombea Rais wetu na taifa letu kwa ujumla,kukemea  hadharani vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi watu" aliongeza Mhe. Ng'wasi.

Awali akisoma taarifa ya Chama  Katibu wa  UVCCM Wilaya ya Iramba  Bw. Amani Daudi amesema zaidi ya vikundi  31 vimenufika na fedha za asilimia 10 za halmashauri ambapo jumuiya ya umoja wa vijana imepata shilingi miloni 207.7.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani (wapili, kushoto) akikabidhi hati ya pongezi kwa umoja wa vijana  wakati wa kikao cha baraza la umoja wa vijana Wilaya ya Iramba, Mkoani Singida Desemba 24, 2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akizungumza na viongozi wa chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida Desemba 24, 2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akisaini Kitabu cha wageni katika Ofisi ya Chama cha Mapinduzi Wilaya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida mara baada ya kuwasili  kwa ajili ya kikao cha baraza la umoja wa vijana Desemba 24, 2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba wakati wa kikao cha baraza la umoja wa vijana wilayani humo Desemba 24, 2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akizungumza na Vijana wa UVCCM Wilaya ya Iramba kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba wakati wa kikao cha baraza la umoja wa vijana wilayani humo Desemba 24, 2025.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Iramba Bi. Emiliana Samson akizungumza wakati wa kikao cha baraza la umoja wa vijana wilayani humo Desemba 24, 2025.

Baadhi ya Vijana wa UVCCM Wilaya ya Iramba wakimsikiliza Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akizungumza kwenye kikao cha baraza la umoja wa vijana wilayani humo Desemba 24, 2025.





DKT. BASHIRU AHIMIZA MJADALA ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka wadau wote wa sekta ya Uvuvi kushirikiana na Serikali kujadili na kupata suluhu kuhusu ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi ikiwa ni pamoja na kukomesha uvuvi usiofuata sheria na taratibu.

Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo Desemba 23,2025 wakati akizungumza na wadau wa sekta hiyo waliopo mwalo wa Kakukuru Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza ambapo ameeleza kuwa katika kipindi cha uongozi wake hatochoma nyavu za Uvuvi au kupima samaki kwa rula kama ilivyokuwa awali.

“Nimemsikia mtu wa “BMU” anataka achome haraka haraka, tunachoma kuna nini humo hata ukizichoma unapata samaki? “Amehoji Balozi Dkt. Bashiru.

Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kuwa kama kutolindwa kwa rasilimali hizo kunaweza kusababisha mgogoro baina ya wavuvi wa dagaa dhidi ya wavuvi wa samaki na wavuvi wa Sangara dhidi ya wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba huku lawama zikielekezwa kuhamia kwa viongozi na watendaji wa Wizara.

Akizungumza kwa niaba ya Wavuvi wenzake kuhusiana na vitendo vya Uvuvi usiofaa Bw. Frank Mwijarobi amesema kuwa hatua za kukabilina na vitendo hivyo zinapaswa kuanza kuchukuliwa na wavuvi wenyewe kutokana na ukweli kuwa rasilimali watu na nyenzo za kudhibiti Uvuvi usiofuata sheria haziwiani na idadi ya watu wanaojishughulisha na vitendo hivyo.

“Mwarobaini ni sisi wenyewe wavuvi kuukataa uvuvi haramu sio viongozi wala makundi ya watu wachache kwa sababu Afisa Uvuvi ni mmoja kwenye kata na ana boti 1 ya doria lakini wavuvi haramu wapo 500 na mbaya zaidi anaishi kwenye nyumba ya mvuvi haramu, anakula kwenye hoteli za Wavuvi haramu anaweza kudhibiti vitendo hivyo?” Ameongeza Bw.Mwijarobi.

Mapema  akiwa kwenye kata ya Maliwanda Wilaya ya Bunda mkoani Mara alikofika kuzungumza na wafugaji wa eneo hilo, Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ndio uti wa mgongo wa uchumi na uhakika wa usalama wa chakula nchini hivyo amewataka wafugaji hao kuendelea kufuga kwa tija wakati Serikali ikiendelea kuboresha mazingira yao ya ufugaji.

Ziara ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru itaendelea Desemba 24,2025 katika mkoa wa Mwanza ambapo anatarajiwa kutembelea kiwanda cha kuzalisha chakula cha samaki na kuzungumza na wavuvi wadogo waliopo mkoani humo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) na timu ya Wataalam wa Wizara yake wakiwasili kwenye visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza tayari kwa kuelekea kwenye kijiji cha Kakukuru kuzungumza na Wavuvi waliopo eneo hilo Desemba 23,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisolya mkoani Mwanza muda mfupi kabla ya kuvuka kuelekea kwenye kisiwa cha Ukerewe Desemba 23,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akizungumza na wadau wa Uvuvi waliopo kwenye kijiji cha Kakukuru Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza Desemba 23,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (aliyevaa shuka la kijani) akikagua mifugo ya kikundi cha Vijana Poa kilichopo kijiji cha Maliwanda mkoani Mara Desemba 23,3025. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji nchini Bw. Murida Mshota.

Jumanne, 23 Desemba 2025

DKT. BASHIRU AALIKA WAWEKEZAJI WA NDANI UFUGAJI SAMAKI KWA NJIA YA VIZIMBA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa nyingi zilizopo kwenye tasnia ya ufugaji wa samaki. 

Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji na wavuvi mkoani Mara Desemba 22,2025 ambapo amewataka wawekezaji hao kuelekeza macho yao kwenye fursa za Viwanda vya vyakula vya samaki, uzalishaji wa vifaranga vya samaki na mikopo kwa vikundi vinavyofanya shughuli hizo za ufugaji wa samaki.

“Ufugaji wa samaki ni utajiri na ndio maana pamoja  na changamoto zilizopo bado hakuna ambaye yupo tayari kuacha kufanya shughuli hiyo hivyo niwaalike wawekezaji hasa wa ndani kwa sababu kwenye eneo la kuzalisha vifaranga tunataka tuwe na wawekezaji ambao watahakikisha vinapatikana wakati wote na wapo ambao kwa uwezo wao wa kimtaji wameshafikia katika hatua mbalimbali” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru amesisitiza kuwa tasnia hiyo ni kielelezo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliiasisi kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi wanawake na vijana kupitia sekta ya Uvuvi hivyo ambapo amewataka watu wote kuchangamkia fursa hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani ambaye alikabidhiwa kusimamia makundi ya vijana na wanawake wanaojihusisha na sekta za Mifugo na Uvuvi amesema kuwa ripoti zinaonesha kuwa kundi la vijana na wanawake wameanza kunufaika na programu hiyo ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ambapo ameahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ili kuendelea kuyanufaisha kiuchumi makundi hayo.

Naye mmoja wa wanufaika wa programu hiyo amesema kuwa wafugaji wote walionufaika na mikopo ya vizimba hivyo katika awamu ya kwanza walifanikiwa kuvuna samaki wengi na kurejesha fedha za mikopo hiyo licha ya changamoto kadhaa walizokumbana nazo kutokana na kukosa uzoefu.

Ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani itaendelea Desemba 23,2025 katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) akiwalisha samaki chakula kwenye eneo la Lake Side mkoani Mara huku akishuhudiwa na baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Wizara yake na Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo Desemba 22,2025.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani wakivuna samaki kutoka kwenye moja ya vizimba vilivyopo kwenye ziwa Victoria eneo la Lake side mkoani Mara Desemba 22,2025.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally kakurwa akiwasalimu wavuvi na wafugaji samaki (hawapo pichani) aliowakuta kwenye eneo la Lake side mkoani Mara Desemba 22, 2025.


Baadhi ya wanawake wanaofanya shughuli za Ufugaji samaki kwa njia ya Vizimba kwenye Ziwa Victoria wakiitikia salamu ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Bashiru Ally Kakurwa (hayupo pichani) alipofika kwenye eneo la Lake side mkoani mara Desemba 22,2025.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa pili kutoka kulia) na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani (kulia) wakiangalia samaki waliowavuna kwenye moja ya vizimba vya kufugia samaki vilivyopo eneo la Lake Side mkoani Mara Desemba 22,2025.

Jumamosi, 20 Desemba 2025

MHE. KAMANI: “WAFUGAJI SHIKANENI MKONO NA SERIKALI KUHUSU MAJI.”

Na. Edward Kondela

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amewataka wafugaji kote nchini kushirikiana na serikali kujenga mabwawa na kuchimba visima ili mifugo iweze kupata maji ya kutosha.

Naibu Waziri Kamani amebainisha hayo (19.12.2025) wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Manyara katika Wilaya ya Hanang, ambapo amewataka wafugaji kuanzia ngazi ya mtu mmoja hadi vikundi kutekeleza hilo badala ya kuisubiria serikali pekee.

Ameongeza kuwa kwa upande wa serikali itaendelea kuweka bajeti ya kujenga mabwawa na kuchimba visima, japokuwa kuna maeneo ambayo vyanzo vya maji viko karibu ambavyo wafugaji wanaweza kujiwekea mkakati wao wenyewe wa kuchimba visima kwa ajili ya maji ya mifugo yao.

Katika hatua nyingine akiwa katika mnada wa Katesh uliopo wilayani humo, ameagiza Bodi ya Nyama nchini (TMB) kufika kwenye mnada huo ili kujiridhisha miundombinu inayotumika katika eneo la machinjio.

Amebainisha hayo baada ya kutoridhishwa na baadhi ya miundombinu, huku akisisitiza ni muhimu kuhakikisha bidhaa ya nyama inayotoka eneo hilo inakuwa salama ili kulinda afya ya mlaji na kufikia malengo ya serikali kufikia zaidi katika masoko ya kimataifa.

Katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Manyara Mhe. Naibu Waziri Kamani amesikiliza maoni na kero mbalimbali ambazo wafugaji wameziwasilisha kwake na kutoa maelekezo ya muda mfupi na muda mrefu.

Baadhi ya kero ambazo zimezungumzwa zaidi na wafugaji ni kuhusu maji, malisho na migogoro ya ardhi, ambapo amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuhakikisha inamlinda mfugaji na mifugo yake na kwamba waendelee kufuata sheria za nchi.

Zawadi ya mavazi maalum ya jamii ya wafugaji kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ndivyo anavyopokea Naibu Waziri Mhe. Ng’wasi Kamani katika Wilaya ya Hanang mkoani Manyara. (19.12.2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani, akivishwa moja ya mavazi maalum ya jamii ya wafugaji katika Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara ikiwa ni sehemu ya heshima kwa kiongozi huyo kuwatembelea wafugaji hao. (19.12.2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani, akizungumza na baadhi ya jamii ya wafugaji (hawapo pichani) katika Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo, huku akiwasisitiza kushirikiana na serikali katika kujenga mabwawa na kuchimba visima. (19.12.2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani (kulia), akipokea zawadi ya ng’ombe (ndama) na mbuzi kutoka kwa jamii ya wafugaji katika Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara. (19.12.2025)

DKT. NCHEMBA AVUTIWA NA VIWANGO BANDARI YA UVUVI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amevutiwa na viwango vya ujenzi wa bandari ya Uvuvi inayokamilishwa ujenzi wake Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.

Mhe. Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa bandari hiyo Desemba 19,2025 ambapo amesema kuwa bandari hiyo ya uvuvi ni mwanzo wa safari ya utekelezaji wa miradi mikubwa iliyoandikwa kwenye DIRA 2050.

"Bandari hii ni mojawapo ya miradi mingi inayofafanua kauli za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizozitoa baada ya kuapishwa kwamba atasimamia utekelezaji wa miradi inayotoa majibu ya kero za Watanzania," Amesema Mhe. Dkt. Nchemba

Aidha Dkt. Nchemba ameongeza kuwa mbali na ujenzi wa bandari hiyo Serikali ipo mbioni kununua meli tano za uvuvi zitakazoongeza kiwango cha mavuno ya samaki ili kuharakisha ukuaji wa sekta ya uvuvi.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema kuwa watahakikisha bandari hiyo inazalisha ajira, mapato na inaendelea kuwa kielelezo cha mafanikio ya Serikali. 

"Kwa vile bandari hii ni ya kisasa, tumeanza mchakato wa kuithibitisha katika viwango vya kikanda na kimataifa hivyo ninawakaribisha wadau kutoka sekta binafsi kwani  wana nafasi kubwa ya kuwekeza kwenye eneo la mafuta (ya boti), viwanda vya uchakataji samaki na uendeshaji wa bandari hiyo.” Amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa bandari hiyo, Msimamizi wa mradi huo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhandisi George Kwandu alimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi huo umefikia asilimia 90 mpaka sasa na utagharimu kiasi cha sh. bilioni 280 hadi kukamilika kwake.

"Mradi huu una eneo la ekari 48. Gati yenye urefu wa mita 315 ambayo ina uwezo wa kupaki meli 10 na zikashusha mzigo kwa wakati mmoja na Jengo hilo likikamilika tutaweza kuhifadhi tani 1.8 za samaki kwa wakati mmoja na kuzalisha tani 100 za barafu kwa siku ambayo ni mahitaji makubwa ya wavuvi kwa sasa.” Ameongeza Mhandisi Kwandu.

Mradi huo unaotarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya Uvuvi nchini unatarajiwa kukamilika na kuzinduliwa mwishoni mwa mwezi Machi 2025.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na baadhi ya mafundi (hawapo pichani) aliokutana nao wakati akikagua hatua za ujenzi wa bandari ya Uvuvi iliyopo Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi Desemba 19,2025. Katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na kulia ni Msimamizi wa Wizara kwenye ujenzi wa Bandari hiyo Mhandisi George Kwandu.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akisalimiana na baadhi ya Viongozi muda mfupi baada ya kuwasili Kilwa Masoko kwenye eneo inapojengwa Bandari ya Uvuvi Desemba 19,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) akimueleza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kulia kwake) fursa zitakazotokana na Bandari ya Uvuvi wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. Nchemba bandarini hapo Desemba 19,2025, Kilwa Mkoani Lindi.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akihutubia wananchi waliofika kwenye eneo inapojengwa bandari ya Uvuvi Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi Desemba 19,2025.

Ijumaa, 19 Desemba 2025

WAFUGAJI WATAKIWA KUWA NA UHAKIKA WA MALISHO YA MUDA MREFU

Na. Edward Kondela

Jamii ya wafugaji katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wametakiwa kuweka malengo ya muda mrefu ya kuwa na maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo yao ili kuondokana na adha ya kuyakosa nyakati za ukame.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amebainisha hayo (18.12.2025) wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja katika wilaya hiyo na kuzungumza na wananchi wa Kata ya Endonyongijape kutokana na hali hiyo ambayo wafugaji wanasema kwa sasa mifugo yao haina malisho ya kutosha.

Mhe. Kamani amewakumbusha wananchi kauli aliyoitoa Waziri wa Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba hivi karibuni, ambapo moja ya sekta inayotakiwa kutazamwa kwa jicho la karibu ni mifugo kutokana na kipindi hiki cha ukame kinachosababishwa na ukosefu wa mvua pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Ameongeza kuwa ni wakati sasa wafugaji kufanya tathmini ya kuwa na maeneo yao na kuhakikisha kuwa na malisho ya kutosha huku serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kusambaza mbegu za malisho hayo kwa wafugaji.

Nao baadhi ya wafugaji katika kata hiyo wamelalamikia madhara ambayo wamekuwa wakiyapata ya uharibifu wa miundombinu mbalimbali na mazao kutokana na uwepo wa tembo na majangili wanaoiba mifugo hali ambayo ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro imekiri kuwepo na tayari imekuwa ikifanyia kazi na kuweka mikakati zaidi ya kuongeza nguvu kuidhibiti.

Aidha, Naibu Waziri Kamani alipata fursa ya kutembelea moja ya mashamba ya wafugaji wakubwa katika wilaya hiyo la Bw. Finias Laizer wa Kijiji cha Langai na kutoa wito kwa wananchi kuiga mfano wa kufuga kisasa na kutumia maeneo makubwa waliyonayo kwa ajili ya kupanda malisho ya mifugo.

Katika ziara hiyo amekuwa akisisitiza juu ya malisho ya mifugo ya kutosha kwa wafugaji ili kuondokana na adha ya kukosa malisho hayo hususan nyakati za ukame.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akiwakumbusha wafugaji katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, kuweka malengo ya muda mrefu ya kuwa na maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo yao ili kuondokana na adha ya kuyakosa nyakati za ukame. (18.12.2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro katika ziara ya kikazi ya siku moja kwenye wilaya hiyo. (18.12.2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akivishwa moja ya mavazi ya kipekee ya kabila la kimaasai mara baada ya kufika katika Kata ya Endonyongijape iliyopo Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ili kuzungumza na wananchi hususan wafugaji. (18.12.2025)

Baada ya kuhitimisha mkutano na wananchi katika Kata ya Endonyongijape iliyopo Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria mkutano huo na kuwaomba kuiombea nchi pamoja na viongozi waliopo. (18.12.2025)

Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani akikagua sehemu ya eneo la kuhifadhia malisho ya mifugo katika shamba la Bw. Finias Kaizer (hayupo pichani) lililopo Wilaya ya Simanjiro mkoani Manayara, ambapo alimshauri mfugaji huyo kuboresha sehemu hiyo ili kutopoteza ubora wa malisho hayo. (18.12.2025)

Jumatano, 17 Desemba 2025

WANAOLIMA MAENEO YA MALISHO, WAONYWA WAONDOKE

Na. Edward Kondela

Wafugaji na wakulima wanaolima kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo wametakiwa kuondoka mara moja kwenye maeneo hayo ili yatumike kama ilivyokusudiwa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amebainisha hayo leo (17.12.2025), wakati wa ziara yake ya kikazi alipozungumza na wananchi wengi wao wakiwa ni jamii ya wafugaji kwenye kongani za malisho katika Kijiji cha Engang’uengare kilichopo Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, baada ya kubainika kuwepo kwa shughuli za kilimo katika maeneo hayo.

Baada ya kusikiliza kero zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa vijiji na wananchi Mhe. Kamani amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada za kudhibiti migogoro ya wakulima na watumiaji wengine wa ardhi huku ikibainika baadhi ya wafugaji kushiriki katika shughuli za kilimo maeneo ya malisho.

Ameongeza kuwa ni wajibu kwa serikali na wafugaji wenyewe kuheshimu na kulinda maeneo ya malisho na wasiwe mstari wa mbele katika kukiuka sheria za nchi.

Katika hatua nyingine Mhe. Naibu Waziri ameshiriki zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa kwa Bw. Sayei Mussa ambaye ni mmoja wa wafugaji wakubwa katika Kijiji cha Orkitikiti na kubainisha kuwa zoezi hilo ni endelevu na kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga Shilingi Bilioni 216 kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kwa ajili ya chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa.

Aidha, ameongeza kuwa chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa ni muhimu katika kuiongezea thamani mifugo hususan kwenye zao la nyama kwa soko la nje ya nchi, hivyo serikali itahakikisha wafugaji wengi wanafikiwa ili kushiriki zoezi hilo muhimu kwa taifa.

Amefafanua kuwa ni muhimu wafugaji kumuunga mkono Mhe. Rais ili kufikia maono ya kutokomeza magonjwa dhidi ya mifugo, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri Wilaya ya Kiteto kwenye chanjo za kimkakati katika wilaya hiyo kwa Mwaka 2024/2025 ng’ombe 184,673 walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu, mbuzi 62,746 dhidi ya ugonjwa wa sotoka na kuku 188,197 dhidi ya ugonjwa wa kideri.

Akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Naibu Waziri Kamani, amearifiwa na mkuu wa wilaya hiyo Bw. Remedius Mwema kwamba ofisi yake imekuwa ikitoa elimu kwa wafugaji kutenga maeneo ya malisho pamoja na kuwachukulia hatua wale wanaovamia maeneo yasiyotakiwa kisheria ili kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Pia, kuhusu chanjo ya utambuzi wa mifugo kitaifa, Bw. Mwema amesema wilaya yake inazidi kuweka mikakati mbalimbali ya kuwafikia wafugaji kutokana na tafiti kuonesha bado baadhi ya wafugaji hawajafikiwa kwa muda unaotakiwa.

Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Manyara, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amekabidhi pikipiki tatu (3) kwa maafisa ugani wa zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa ili kuongeza wigo wa kuwafikia wafugaji wengi zaidi.

Katika maeneo mbalimbali ya ziara yake, Mhe. Naibu Waziri Kamani amepokea maoni ya wananchi hususan wafugaji kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji ya kutosha, majosho na mbegu za malisho huku akiahidi serikali kuendelea kutatua changamoto hizo kwa kushirikiana na wananchi.

Chanjo ya mifugo kitaifa inaenda sambamba na utambuzi wa mifugo kwa kuwekewa hereni za kieletroniki, ambapo akiwa katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani ameshiriki kumuwekea mbuzi hereni. (17.12.2025)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani, akisoma maelezo kwenye chupa ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu (CBPP) baada ya kufika kwa mmoja wa wafugaji wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, kushuhudia zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa katika wilaya hiyo. (17.12.2025)

Zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa, likishuhudiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani (kushoto) alipotembelea na kushuhudia utekelezaji wa zoezi hilo katika Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara. (17.12.2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani (mwenye nguo ya kijani) akiwa na baadhi ya maafisa kutoka wizarani na Wilaya ya Kiteto, pamoja na mkuu wa wilaya hiyo Bw. Remedius Mwema kulia kwake, baada ya kukabidhi pikipiki tatu (3) kwa maafisa ugani wa zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo katika wilaya hiyo, mkoani Manyara. (17.12.2025)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani, amewataka wafugaji na wakulima wanaofanya shughuli za kilimo kwenye maeneo ya malisho ya mifugo kuondoka mara moja na kuyaacha maeneo hayo kwa matumizi yaliyokusudiwa. Mhe. Kamani amebainisha hayo katika ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara. (17.12.2025)




DKT. BASHIRU AONGEZA MSUKUMO KWENYE MAPATO UVUVI WA BAHARI KUU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa bahari kuu (DFSA) kuongeza kiwango cha makusanyo ya mapato yatokanayo na Uvuvi wa Bahari Kuu.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameyasema hayo mara baada ya kufika na kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Mamlaka hiyo Desemba 17,2025 visiwani Zanzibar ambapo mbali na kuwapongeza kwa kuanza kuongeza kiwango cha makusanyo amewataka kuhakikisha wanakusanya zaidi ya fedha zinazokusanywa kwenye shughuli nyingine za Uvuvi.

“Mhe. Rais hapendi michakato, anataka matokeo na nyie wenyewe mliona namna ile filamu ya Royal tour ilivyofanya mapinduzi ya sekta ya Utalii hivyo na nyie mfikirie mpango utakaofanya mapinduzi kwenye Uvuvi wa bahari kuu” Ameongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Dkt. Bashiru ameitaka Mamlaka hiyo kuweka mikakati madhubuti itakayoainisha ushiriki wa sekta binafsi kwenye Uvuvi wa bahari kuu huku akizipongeza baadhi ya sekta zilizoanza kuwekeza kwenye eneo hilo.

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Masoud Ally Mohammed amesema kuwa anaamini ziara hiyo ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Makatibu Wakuu wa Wizara zote mbili itakuwa chachu ya utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyojikita kwenye kuhakikisha uchumi wa Tanzania unachagizwa kwa kiasi kikubwa na Uvuvi wa bahari kuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Salehe Yahya amesema kuwa Mamlaka yake itahakikisha inaongeza pato la Taifa kupitia uchumi wa Buluu huku akibainisha kuwa uchumi huo utaongezeka kwa kiasi kikubwa zaidi mara baada ya kuanza kufanya kazi kwa Mashirika ya Uvuvi Tanzania bara (TAFICO), lile la Zanzibar (ZAFICO) na bandari ya Uvuvi inayokamilishwa ujenzi wake wilayani Kilwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) akiwa ameshikilia matango bahari aliowakuta wakifugwa kwenye kampuni ya kuendeleza ukuzaji viumbe maji iliyopo eneo la Betrasi visiwani Zanzibar Desemba 17,2025. Kulia ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Masoud Ally Mohammed.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi kutoka Zanzibar Mhe. Masoud Ally Mohammed (kulia) akimueleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) mikakati ya Wizara yake kwenye kukuza uchumi wa Buluu muda mfupi baada ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru kuwasili ofisini kwake visiwani Zanzibar Desemba 17,2025. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena.

Kaimu Meneja Kitengo cha Udhibiti wa Uvuvi wa Bahari kuu Bw. Daniel Pius Kawiche (kulia) akimueleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kushoto), Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Masoud Ally Mohammed (wa pili kutoka kushoto) na Watendaji wa Wizara hizo mifumo ya kisasa inayotumika kuratibu shughuli za Uvuvi wa bahari kuu wakati za Ziara ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Visiwani humo Desemba 17,2025.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) Dkt. Saleh Yahya (kulia) akimfafanulia Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kushoto), Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Masoud Ally Mohammed (wa pili kutoka kushoto) namna wanavyokusudia kuongeza mapato yatokanayo na Uvuvi wa Bahari Kuu wakati za Ziara ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Visiwani humo Desemba 17,2025.

Jumanne, 16 Desemba 2025

DKT. BASHIRU AAGIZA MAMBO 6 KATIKA KUTEKELEZA MRADI WA MAZIWA NCHINI

Na. Hamisi Hussein, Dodoma 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally, ameiagiza timu ya wataalam wanaotekeleza Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi kuzingatia maeneo sita muhimu yatakayowezesha utekelezaji wenye tija na kwa wakati mradi huo nchini.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ametoa maelekezo hayo leo, Desemba 16, 2025, katika Ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mtumba jijini Dodoma, wakati wa kikao cha kupitia mwenendo wa utekelezaji wa mradi huo, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuzingatia upatikanaji wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa, upatikanaji wa maji katika maeneo yanayotekelezwa mradi, utambuzi sahihi wa wanufaika, upatikanaji wa malisho kwa wafugaji, pamoja na usimamizi na uratibu unaojumuisha wadau wote wa sekta ya mifugo.

" Mfanye uratibu kwa makini kupata  mbegu za bora za ng'ombe wa maziwa, malisho na maji ili hii tasnia ilete tija" Alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aliongeza kuwa wataalam wanaosimamia mradi huo kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia ya kisasa ili kuendana na kasi ya dunia katika kuongeza tija na thamani ya tasnia ya maziwa nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani, alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo unapaswa pia kuzingatia kuwahusisha wataalam ili kutathmini fursa za ufugaji wa mbuzi wa maziwa kwa wanawake na vijana, hatua itakayopanua wigo wa ajira na kuongeza mchango wa makundi hayo katika tasnia ya maziwa.

Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Mratibu wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi, Dkt. Lazaro Kapella, alisema mradi unagharimu dola za Marekani milioni 229.982 na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi na kueleza kuwa takribani wananchi 700,000 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo unaotekelezwa katika mikoa nane ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Stephen Michael, alibainisha kuwa ucheleweshaji wa utoaji wa fedha kutoka kwa baadhi ya wafadhili umeathiri utekelezaji wa baadhi ya shughuli za mradi kwa wakati uliopangwa.

Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi unafadhiliwa na wadau mbalimbali wakiwemo IFAD, OPEC Fund, GCF, AFD, TADB, HI, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wanufaika wa mradi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally akizungumza wakati alipoongoza  Kikao cha wasilisho la Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiriko ya Tabia ya Nchi,  kilichofanyika Desemba 16, 2025 Ukumbi wa Wizara uliopo Mtumba,  Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi  Kamani, akitoa mapendekezo ya ushirikishwaji wa Wanawake na Vijana katika tasnia ya maziwa wakati wa kikao cha wasilisho la Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiriko ya Tabia ya Nchi, kilichofanyika Desemba 16, 2025  Ukumbi wa Wizara uliopo Mtumba, Jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally (wa tano kushoto) akitoa maelekezo kwa timu ya wataalam wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi,  wakati wa Kikao cha wasilisho la mradi huo kilichofanyika, Desemba 16, 2025 Ukumbi wa Wizara uliopo Mtumba Jijini Dodoma. Wa tano kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Kamani.

Mratibu wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi, Dkt. Lazaro Kapella, akitoa taarifa kuhusiana na hali ya utekelezaji wa mradi wakati wa kikao cha wasilisho  kilichofanyika Desemba 16, 2025 katika Ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi uliopo Mtumba, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya  Uzalishaji na Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Stephen Michael (wa kwanza kulia), akielezea hatua zilizofikiwa katika Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiriko ya Tabia ya Nchi, katika Kikao cha wasilisho la Mradi huo kilichofanyika Desemba 16, 2025 katika Ukumbi wa Wizara uliopo Mtumba, Jijini Dodoma.

Jumatatu, 15 Desemba 2025

TALIRI YATAKIWA KUFANYA TAFITI ZENYE KUONGEZA THAMANI YA MIFUGO MASOKO YA NJE YA NCHI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuhakikisha tafiti zake zinalenga kuongeza thamani ya mazao ya Mifugo ili kukidhi masoko ya nje ya Nchi.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo aliyoifanya Desemba 15, 2025 jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ulioelekeza ufugaji wa kisasa, kibishara na wenye tija.

“Mimi niwaombe mambo matatu, la kwanza tafiti zenu zielekezwe katika kuongeza thamani ya mazao ya Mifugo na hasa katika kuuza zaidi kwenye soko la nje ili mauzo yaongezeke kutoka tani elfu 14 kwa sasa hadi tani elfu 50 ifikapo mwaka 2030” Ameongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Vilevile Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameitaka taasisi hiyo kufanya tafiti zinazohusu uhimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi ambapo amesisitiza ushirikiano wa kitafiti wa Taasisi za Wizara yake na ile ya Maji ili kuboresha eneo la malisho ya Mifugo na Maji.

“Jambo la tatu ni mkakati wa kuendeleza sekta ya ufugaji wa kuku kwa sababu tunataka tubadilishe sekta hiyo hapa nchini na kwenye hili tuwafate wafugaji walipo ili kutatua changamoto zao kwani wanafanya kazi kubwa hususani vijana na akina mama” Amehitimisha Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Erick Komba amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Balozi Dkt. Bashiru yapo kwenye miongozo mbalimbali ya utekelezaji wa shughuli za kitafiti hivyo ameahidi yeye pamoja na timu yake kufanyia kazi maelekezo hayo.

“Yote yaliyoelekezwa ni mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu na tuna utaalamu hivyo tutahakikisha tunayafanyia kazi ili juhudi za Mhe. Rais Samia, malengo na Wizara na Taasisi yaweze kutimia lengo likiwa ni kuongeza kipato cha mfugaji na pato la Taifa kwa ujumla” amesema Prof. Komba.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Vitus Komba (wa pili kulia) akielezea teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na taasisi hiyo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa tatu kulia) aliyembatana na Viongozi wengine wa Wizara waliotembelea Taasisi hiyo Leo tarehe 15/12/2025 kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na TALIRI.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa kwanza kutoka kushoto) akisalimiana na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Desemba 15, 2025 alipotembelea Taasisi hiyo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na taaisisi hiyo na watumishi hao. Katika ziara hiyo Mhe. Waziri ameongozana na Viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ng’wasi Kamani, Katibu Mkuu Bi. Agnes Meena na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Edwin Mhede.

Mkurugenzi Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Komba (wa kwanza kulia) akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za Taasisi mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb) (wa nne kulia) wakati alipotembelea TALIRI leo tarehe 15/12/2025 kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo pamoja kuongea na watumishi.

Menejimenti ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa katikati) mara baada ya kuongea na watumishi wa taasisi hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Waziri ya kutembelea Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo lengo ikiwa ni kuona namna shughuli za Taasisi hizo zinatekelezwa.