Na. Edward Kondela
Jamii ya wafugaji katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wametakiwa kuweka malengo ya muda mrefu ya kuwa na maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo yao ili kuondokana na adha ya kuyakosa nyakati za ukame.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amebainisha hayo (18.12.2025) wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja katika wilaya hiyo na kuzungumza na wananchi wa Kata ya Endonyongijape kutokana na hali hiyo ambayo wafugaji wanasema kwa sasa mifugo yao haina malisho ya kutosha.
Mhe. Kamani amewakumbusha wananchi kauli aliyoitoa Waziri wa Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba hivi karibuni, ambapo moja ya sekta inayotakiwa kutazamwa kwa jicho la karibu ni mifugo kutokana na kipindi hiki cha ukame kinachosababishwa na ukosefu wa mvua pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa ni wakati sasa wafugaji kufanya tathmini ya kuwa na maeneo yao na kuhakikisha kuwa na malisho ya kutosha huku serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kusambaza mbegu za malisho hayo kwa wafugaji.
Nao baadhi ya wafugaji katika kata hiyo wamelalamikia madhara ambayo wamekuwa wakiyapata ya uharibifu wa miundombinu mbalimbali na mazao kutokana na uwepo wa tembo na majangili wanaoiba mifugo hali ambayo ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro imekiri kuwepo na tayari imekuwa ikifanyia kazi na kuweka mikakati zaidi ya kuongeza nguvu kuidhibiti.
Aidha, Naibu Waziri Kamani alipata fursa ya kutembelea moja ya mashamba ya wafugaji wakubwa katika wilaya hiyo la Bw. Finias Laizer wa Kijiji cha Langai na kutoa wito kwa wananchi kuiga mfano wa kufuga kisasa na kutumia maeneo makubwa waliyonayo kwa ajili ya kupanda malisho ya mifugo.
Katika ziara hiyo amekuwa akisisitiza juu ya malisho ya mifugo ya kutosha kwa wafugaji ili kuondokana na adha ya kukosa malisho hayo hususan nyakati za ukame.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni