Na. Stanley Brayton
◼️Wazishukuru pia Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kudhamini Vifaa vya Michezo.
Mwenyekiti wa Wanamichezo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Sebastian Shilangalila kwa niaba ya wanamichezo, amemshukuru kwa dhati Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Agnes Meena kwa kuwezesha wanamichezo wa Wizara hiyo kushiriki katika Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) Mkoani Mwanza.
Akizungumza katika Hafla fupi ya kupongezana na kupata Chakula cha pamoja katika Ukumbi wa Maabara ya Uvuvi Nyegezi - Mwanza, leo Septemba 11, 2025, Bw. Shilangalila amesema Timu ya wanamichezo toka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imeshiriki katika Michezo mbalimbali na imefanikiwa kufika katika hatua kubwa mbalimbali ikiwemo Mchezo wa kamba kwa Wanaume kuingia nusu fainali na Timu ya Ikulu, na hii yote ni kutokana na mchango Mkubwa wa Katibu Mkuu, Bi. Agnes Meena.
“Katibu Mkuu wetu ametuwezesha fedha za kushiriki katika Michuano ya SHIMIWI, na pia siku kama ya leo katupatia kilo 100 za Samaki kwa ajili ya chakula cha pamoja cha wanamichezo, na kiasi cha shilingi Milioni Moja kama motisha kwa wanamichezo ili kuongeza hali na nguvu zaidi.” Amesema Bw. Shilangalila
Aidha, Bw. Shilangalila amezishukuru Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa ufadhili wa Vifaa vya Michezo na vitu vingine, ikiwemo Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Kampuni ya Ranchi za Kitaifa (NARCO), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Kitengo cha Ulinzi na Usimamizi wa Raslimali za Uvuvi (FRP) - Mwanza, Kitengo cha Udhibiti Ubora na Masoko ya Mazao ya Uvuvi (QC) pamoja na aliyekuwa Meneja wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Nyegezi, Bw. Stephen Lukanga.
Naye, aliyekuwa Meneja wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Nyegezi, Bw. Stephen Lukanga amewapongeza wanamichezo wote na kuwapatia motisha ya katoni 15 za maji ya kunywa ambazo zitawasaidia wanamichezo katika Michezo, na pia amewatia moyo katika Michezo inayoendelea.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni