Nav bar

Jumanne, 10 Mei 2022

​SERIKALI YATUMIA ZAIDI YA MILIONI 300 KUNUNUA BOTI ZA UVUVI

Serikali imenunua boti 16 na injini 12 zenye thamani ya Sh Milioni 395 ambazo zitatumiwa na maafisa uvuvi katika kudhibiti  rasilimali za uvuvi nchini.


Hayo yamesemwa Aprili 30, 2022  jijini Mwanza na  Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi boti  kwa maafisa wafawidhi wa uvuvi kwa kanda za Ziwa Victoria,  Tanganyika, Kanda ya Bahari ya Hindi, Kaskazini Mashariki  na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.  


Waziri Ndaki amesema  kuwa boti na injini hizo zimenunuliwa na Serikali ili kuiwezesha Wizara na watalaam wake kutekeleza jukumu lake la msingi la kusimamia, kulinda na kuendeleza Rasilimali za uvuvi nchini.


Amesema mbali na Serikali kununua vifaa hivyo ameziomba Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kununua vifaa hivyo ili kudhibiti rasilimali za uvuvi dhidi ya watu wanaojihusisha na uvuvi haramu.


“ Halmashauri zetu zilizo kwenye mwambao wa bahari/ziwa na mito zishirikiane na Wizara ili kwa pamoja tudhibiti uvuvi haramu ambao bado ni changamoto kwa sasa”, alisema Mhe. Ndaki


Ameongeza kuwa Serikali itawashughulikia wavuvi haramu wote na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.


Waziri Ndaki amewataka wavuvi nchini kuhakikisha kuwa wanalinda rasilimali za uvuvi ili zisiharibiwe  na watu wanaojihusisha na shughuli za uvuvi haramu.


Pia amewataka maofisa uvuvi waliokabidhiwa boti na injini hizo kuhakikisha kuwa wanazilinda na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.


Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema shughuli za uvuvi nchini hufanyika katika maji baridi na maji bahari na kwa kiasi kikubwa zikihusisha wavuvi wadogo.


Dkt. Tamatamah amesema katika mwaka 2021 wavuvi wadogo wapatao 194,804 walishiriki moja kwa moja katika shughuli za uvuvi kwa kutumia vyombo vya uvuvi vipatavyo 57,991 na kuwezesha kuvuna tani 477,019 za samaki zenye thamani ya shilingi trilioni 2.8 ambapo tani 302,827.9 sawa na asilimia 63.0 zilitoka Ziwa Victoria.


Aliongeza kuwa uvuvi huo ulihusisha pia  kiasi cha tani 42,302 na samaki hai wa mapambo 181,268 zenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 414.23.


“Kati ya tani za samaki zilizosafirishwa kwenda nje ya nchi, tani 36,657.46 sawa na asilimia 86.7 zilitoka Ziwa Victoria,” alisema Dkt. Tamatamah


Dkt. Tamatamah amefafanua kuwa ili uzalishaji wa samaki pamoja na mapato yake kwenye ziwa hili yawe endelevu, ajira zinazotokana na shughuli za uvuvi kwenye ziwa ziwe endelevu, miundombinu ya uvuvi iliyowekezwa na serikali na watu binafsi iweze kufanya kazi kwa muda mrefu na manufaa yatokanayo na shughuli za uvuvi kwenye ustawi wa jamii yawe endelevu, wananchi hawana budi kulinda na kuzisimamia ipasavyo rasilimali za uvuvi pamoja na mazingira zinakofanyika shughuli za uvuvi.


Amesema katika juhudi za Wizara kusimamia rasilimali za uvuvi,  iliunda Kanda kuu nne za usimamizi wa rasilimali za uvuvi ambazo ni Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya Ziwa Tanganyika, Kanda ya Bahari ya Hindi na Kaskazini Mashariki na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zenye jumla ya vituo 36 vya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Wizara ya Mifugo na uvuvi kwa hatua hiyo ya kununua vifaa hivyo ambavyo vitasaidia katika kudhibiti na kupambana na wavuvi haramu mkoani Mwanza na nchini kwa ujumla.


Akitoa shukurani kwa niaba ya maafisa ufawidhi wa uvuvi walipokea vifaa hivyo, Afisa Mfawidhi kutoka Kanda ya Bahari Hindi na Kaskazini Mashariki Mathayo Werema ameishukuru Serikali kwa ununuzi wa vifaa hivyo ambavyo watavitumia katika kudhibiti, kulinda rasilimali za uvuvi, lakini pia kutoa elimu kwa jamii kuondokana na vitendo vya uvuvi haramu.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akiwa kwenye moja ya boti za doria zilizogaiwa  kwa maafisa wafawidhi kuona ubora wake namna litafanya kazi, kushoto ni Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, April 30, 2022 Jijini Mwanza


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiongea na maafisa wafawidhi (hawapo pichani) Mkoani Mwanza, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi boti za doria 16 na injini 12, na kuwasihi kuzitumia kwa kazi iliyokusudiwa na sio vinginevyo. Aprili 30, 2022 kwenye eneo la kisiwa cha sanane Mkoani Mwanza.



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah akiongea na maafisa wafawidhi (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya kukabidhi boti za doria 16 na injini 12 na kuwataka kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na Sheria  Aprili 30,2022 Jijini Mwanza.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (kulia) akiwasili kwenye eneo lililoandaliwa kwa ajili kukabidhi boti za doria kwa maafisa wafawidhi lengo likiwa ni pamoja na kutunza, kusimamia na kuhifadhi rasilimali za uvuvi Nchini. Aprili 30, 2022.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akizindua zoezi la kukabidhi boti 16 na injini 12 kwa maafisa wafawidhi kwa kukata utepe Aprili 30, 2022 Jijini Mwanza.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb)(wa nne kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakuu wa vituo vya doria, na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi, wa tatu kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi, na wa tano kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah. Aprili 30, 2022 Jijini Mwanza.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni