Nav bar

Jumanne, 10 Mei 2022

KATIBU MKUU MIFUGO ATEMBELEA MINADA YA UPILI JIJINI ARUSHA.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda amefanya ziara ya kutembelea Minada ya Upili inayosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) kwa lengo la kuangalia kazi mbalimbali zinazotekelezwa katika minada hiyo.


Aidha, Minada aliyotembelea ni pamoja na Mnada wa Mpakani wa Longido, Miserani na Themi.Vilevile, Nzunda alipata fursa ya kutembelea Kiwanda cha nyama cha ELIYA FOOD OVERSEAS LTD na bwawa la Kimokouwa lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Longido.


Katika hatua nyingine, Afisa Mifugo wa Wilaya ya Longido Bw.Nestory Dagharo alimweza katibu Mkuu Mifugo kuwa shughuli kuu ya wakazi wa Wilaya hiyo ni  ufugaji, hivyo wameweza kuboresha Mifugo kwa maana ya ng'ombe na Mbuzi kwa asilimia 40 na wameweza kuwajengea wafugaji mazizi ya Chuma 60 na kwa sasa wanaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa mazizi ya 1,700 kwa msaada wa mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali ya World Wide Fund (WWF) na Tanzania People's and Wild Life (TPW)


Dagharo alisema kuwa kutokana na Mabadiliko ya Tabia nchi yaliyotokea Mwaka jana ya Ukame ambayo yaliathiri Mifugo kwa kufa kwa Wingi baadhi ya sehemu kwa kukosa malisho na Maji, uongozi wa Wilaya ya Longido umechukua hatua ya kutoa elimu kwa wafugaji kuzalisha Malisho kwa  kuanzisha Mashamba Darasa ya Malisho ili wafugani waweze kujifunza.


Dagharo aliongeza kuwa, Wilaya hiyo imeweza kukarabati Majosho 2 katika kijiji cha Ngereyani na bwawa moja lilikarabatiwa katika kijiji cha Lesing'ita na moja lilichimbwa katika kijiji cha Olmolog.


"Kwa sasa Mvua zimeanza kunyesha kidogo na Malisho yameanza kuota kwahiyo wafugaji wetu hawana shida sana ya Malisho.Vilevile soko la Mifugo lipo, wafugaji wetu wanapeleka Mifugo yao kuuza katika kiwanda cha Eliya Food Overseas LIMITED".Alisema Dagharo.


Kwa Upande wake Katibu Mkuu Mifugo alielekeza Uongozi wa Wilaya ya Longido kuwahimiza Wafugaji kubadilika,kwa sababu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) imeandaa Mpango Mkakati wa Mabadiliko ya Sekta ya Mifugo wa Miaka 5 ikiwemo uboreshaji wa Mbali za Mifugo nchini.


Pia, Nzunda alisema kuwa Mpango Mkakati huo wa Mabadiliko ya Sekta ya Mifugo umezingatia Uchimbaji wa Mabwawa kwa ajili ya Mifugo, wafugaji watatakiwa kuzalisha Malisho kwa ajili ya Mifugo yao, kuchanja na kuogesha Mifugo.


"Kwa sasa suala la Afya ya Mifugo haliepukiki, kuchanja, kuogesha Mifugo sio jambo la hiari tena, tuna magonjwa ya Mifugo13 ambayo tusipoyadhibiti Mifugo yetu haiwezi kuuzika nje ya nchi, tutakosa masoko ya mazao ya Mifugo kimataifa,hivyo tutakuwa tumejiwekea vikwazo vya kiuchumi sisi wenyewe, kwahiyo wafugaji lazima wachanje,waogesha Mifugo yao".Alisema Nzunda.


Nzunda alibainisha kuwa sasa ni wakati wa kubadilisha fikra za wafugaji, Ufugaji wa kuchunga umepitwa na wakati, Mifugo inaongezeka, Binadamu wanaongezeka,lakini ardhi haiongezeki,wafugaji waondokane na fikra kuwa wao ni maskini, wao ni wawekezaji,wafuge kisasa na wavune mifugo yao ili iwaletee tija.


Aidha, Katibu Mkuu Mifugo alisema kuwa Serikali imetafuta Masoko ya nje ya kuuza Mazao ya Mifugo ikiwemo nyama, lakini changamoto kubwa iliyopo hakuna nyama ya kupeleka katika masoko hayo, Mifugo yetu hapa Tanzania haina sifa ya nyama ya kwenda huko katika soko la nje.


"Tanzania ni nchi ya pili Africa kuwa na Mifugo Mingi ikitanguliwa na Ethiopia, lakini Mifugo hiyo haichangii asilimia kubwa katika pato la Taifa.Sasa tunafikiria kuingi kwenye mfumo wa E-service ili ng'ombe wetu wauzwe kwenye mfumo kiasi kwamba mteja atakuwa na uwezo wa kununua ng'ombe hata akiwa nje ya nchi".Alisema Nzunda.


Vilevile Katibu Mkuu Mifugo alionya watumishi wasiokuwa waadilifu wanaoshirikiana na wafanyabiashara kutorosha Mifugo kwenda nchi jirani bila kufuata utaratibu, alisema kuwa mtumishi yeyote atakayebainika anafanya hivyo taratibu,kanuni na sheria za kiutumishi zitachukuliwa dhidi yake.


Awali Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Nurdini Babu alisema kuwa wafugaji wengi wanatorosha Mifugo kwenda nchi jirani wanadai kuwa  hapa kwetu Tanzania tozo na Ushuru ni mkubwa kuliko nchi jirani, hivyo Wizara iangalie namna bora ya kuweza kushusha hizo tozo. 


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longido Bw.Simon Oitesoi amesema  kuwa ni kweli utoroshaji wa Mifugo kwenda nchi jirani unafanyika kwa kiwango kikubwa,hivyo Halmashauri inaendelea kutoa elimu kwa Wafugaji ingawa utoroshaji huo unachangiwa na Watumishi wasiokuwa Waadilifu.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda (wa Pili kutoka kulia) akiwa katika mnada wa Upili wa Miserani katika halmashauri ya Wilaya ya Monduli akikagua ujenzi wa Ukuta wa Mnada huo. Kutoka kulia ni Raphael Mwampashi,Afisa Mfawidhi Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo (ZVC) kanda ya kaskazini Arusha, James Elikunda, Mkandarasi aliyejenga ukuta  mnadani hapo,Wengine ni watumishi katika Mnada huo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni