Nav bar

Jumanne, 8 Julai 2025

WAFUGAJI MKOANI SINGIDA WAHAMASISHWA KUCHANJA NA KUTAMBUA MIFUGO YAO

Na Chiku Makwai, Singida

Wafugaji mkoani Singida wametakiwa Kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchanjaji na utambuzi wa Mifugo yao ambapo utekelezaji wa zoezi hilo mkoani humo limeanza leo  Julai 8, 2025 katika Kijiji cha  Makunda kilichopo wilayani Iramba lengo likiwa ni kuikinga mifugo yao dhidi ya magonjwa na kuiboresha  kwa ajili ya Soko la Kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt. Pius Mwambene  amesema zoezi hilo ambalo limeziduliwa mwezi June 16, 2025, na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan litaongeza tija kwa wafugaji kote nchini hivyo wanapaswa Kulizingatia.

Dkt. Mwambene amesema kuwa katika Kampeni ya Chanjo ambayo inaendelea nchini wafugaji watachanja mifugo yao kwa bei ya ruzuku baada ya Serikali kutoa bilioni 216 fedha za kitanzania kwa ajili ya zoezi hilo ambalo litafanyika kwa miaka mitano.

"Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alishazindua kampeni hii ya chanjo na ameridhia kuchangia nusu gharama ya chanjo ili kuwasaidia wafugaji kote nchini kuikinga mifugo yao dhidi ya magonjwa na kuimarisha biashara ya Mifugo na mazao yake katika masoko ndani na Kimataifa, hivyo wafugaji wa mkoa huu wa Singida jitokezeni na mshiriki kikamilifu kwenye kampeni hii" alisema Dkt. Mwambene.

Baadhi ya Wafugaji Wilayani Iramba wameishukuru Serikali kwa Kuwashika Mkono katika Chanjo ya Mifugo wakisisitiza kuwa Kabla ya Chanjo hiyo mifugo mingi imekuwa ikifa kutokana na Magonjwa Mbalimbali.

Utekelezaji wa zoezi hilo ulioenda sambamba na uhamasishaji wa wafugaji kushiriki kikamilifu kampeni hiyo  umefanyika leo Julai 8, 2025 katika Kijiji cha Makunda Wilayani Iramba Mkoa wa Singida na Mifugo zaidi ya Milioni 1 inatarajiwa kupewa chanjo mkoani humo.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni