Nav bar

Alhamisi, 10 Juni 2021

SERIKALI KUFUTA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI KWENYE VIFAA VYA UVUVI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalla Ulega amesema Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vingi vya uvuvi ikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu, nyavu za uvuvi na vifungashio ili kuwasaidia wavuvi kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu.

Mhe. Ulega aliyasema hayo Juni 09, 2021, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Sylivia Sigula ambaye alitaka kufahamu mpango wa Serikali katika kuwawezesha wavuvi wa Ziwa Tanganyika wavue kisasa ili kupata kipato Zaidi na kutoa ajira kwa vijana.

"Kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2011 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato ya mwaka 2014, Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vingi vya uvuvi ikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu, nyavu za uvuvi na vifungashio ili kuwasaidia wavuvi kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu," alisema Mhe. Ulega

Alisema kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ili wavuvi wapate mikopo ya masharti na riba nafuu kutoka katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) na kupitia Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali (TIB). 

Aliongeza kuwa Wizara kupitia Dawati la Sekta Binafsi imeviunganisha vyama vya ushirika vya wavuvi na taasisi za fedha ambapo mikopo iliyoombwa na kupitishwa ni shilingi bilioni 2.6 na mikopo iliyotolewa ni shilingi milioni 560.7. 

“Wizara imehamasisha Benki ya Posta (TPB) kuanzisha na kuzindua Akaunti ya Wavuvi (Wavuvi account) kwa ajili ya mikopo na bima mahususi kwa wavuvi hususan wavuvi wadogo. “ Alisema Mhe. Ulega 

Aidha, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wavuvi kufanya uvuvi wenye tija na kuwahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na VICOBA ili waweze kukopesheka kwa urahisi na taasisi za fedha na hivyo kujikwamua kiuchumi.  

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Sylivia Sigula aliyetaka kufahamu kauli ya Serikali kwa vijana ambao wamejiunga kwenye vikundi na wamekidhi vigezo lakini hawajapatiwa vifaa vya kuvulia na mikopo, Mhe Ulega alisema juu ya mafunzo na uwezeshaji wa vijana yaliyokwisha kuanzishwa, kuna chuo cha uvuvi kilichopo kigoma mjini, tutahakikisha chuo kile kinafikia makundi yote  na aliomba Mhe. amuwasilishie vikundi vya ziwa Tanganyika kimoja baada ya kingine ili kuweza kuvifikia na kuviwezesha.

Aliongeza kuwa, Serikali hususan Wizara ya Mifugo na Uvuvi, tulifanya jitihada za makusudi za kuanzisha dawati la sekta binafsi na sasa limefanya kazi kubwa na kabla ya kuanzishwa kwa dawati idara ya uvuvi ilipata mikopo sawa na asilimia sifuri kwa wavuvi wadogo na baada ya kuanzishwa tumeipandisha hadi kufikia milioni mia tano na sitini.

Mkakati wetu ni kuhakikisha tunaimarisha Zaidi dawati la sekta binafsi kimkakati kwa ajili ya kuiwezesha sekta hii kupata pesa Zaidi.

“maandiko ya vikundi hivi vya wavuvi wetu tutayapitia na kuwawezesha waweze kuwashawishi benki kuweka pesa Zaidi." Alisema Mhe. Ulega.

Aliongeza kuwa dawati la sekta binafsi limefika pazuri na shirika la bima la Taifa linakwenda kutupelekea kupata bima ya wavuvi na bima ya mifugo ili mabenki yaweze kuwa na hamu ya kutoa pesa Zaidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni