Nav bar

Jumatano, 16 Desemba 2020

WAZIRI MASHIMBA ATOA MAAGIZO 3 KUDHIBITI HOMA YA MAPAFU KWA NG’OMBE

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amemuagiza Kaimu Meneja Mkuu, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Maselle Shilagi kuhakikisha anawapa chanjo Ng’ombe wote katika Ranchi 14 za Taifa ili kuwakinga na ugonjwa wa homa ya mapafu ulioanza kuathiri baadhi ya Ng’ombe katika Ranchi ya Kongwa.

 

Ndaki alitoa agizo hilo Disemba 11, 2020 alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ranchi ya Kongwa iliyopo Mkoani Dodoma baada ya kupata taarifa ya mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu katika Ranchi hiyo.

 

Alisema kwasababu ugonjwa huo umekuja kwa ghafla hakuna haja ya kusubiri jitihada za haraka zichukuliwe kuudhibiti mapema kabla haujasambaa katika maeneo mengine na kusababisha madhara makubwa zaidi.

 

“Kwa kuwa tayari tuna dozi 9500 za chanjo ambazo zimefika hapa, namuagiza Kaimu Mkurugenzi ahakikishe anaanza kuwapatia chanjo ng’ombe hawa kuanzia leo na kufika kesho saa saba mchana nipate taarifa ya maendeleo ya uchanjaji kwa sababu ni jambo la dharura hivyo hatuwezi kusubiri sana, ili kama kuna mabadiliko mengine tuweze kuona ni hatua gani zinachukuliwa,” alisema Ndaki

 

Aliongeza kwa kusema kuwa hali ya ng’ombe katika ranchi hiyo bado ni nzuri na wakianza kupewa chanjo leo ugonjwa huo utadhibitiwa huku akiwataka kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kuchanja ng’ombe wote waliopo katika Ranchi nyingine ili ugonjwa usiathiri afya za mifugo.

 

“Nafahamu kuwa katika hizi Ranchi pia wapo ng’ombe wa wafugaji binafsi, natoa maelekezo kuwa ng’ombe hao pia wapatiwe chanjo pamoja na ng’ombe wa maeneo ya jirani kwa sababu tukichanja ng’ombe wa kwetu tukaacha hao wengine tutakuwa hatujatibu tatizo,” alisisitiza Ndaki

 

Aidha, Ndaki alitumia fursa hiyo kuwaondoa hofu wafugaji wote waliopo katika maeneo ya Kongwa na sehemu nyingine kuwa wasiwe na wasiwasi kwa sababu serikali imeshaleta chanjo na zoezi la uchanjaji litaanza mara moja kudhibiti ugonjwa huo.

 

Kwa upande wake, Daktari wa Mifugo, Ranchi ya NARCO Kongwa, Dkt. Nickson Mbise alisema toka ugonjwa huo ulipoanza kuathiri Wanyama mpaka sasa wameshakufa ng’ombe watano (5) kati ya ng’ombe 9200 waliopo katika ranchi hiyo huku akisema chanzo kikubwa cha vifo hivyo ni homa ya mapafu.

 

 “Dalili za mwanzo tulizoziona ni ng’ombe kupumua kwa shida na wakati mwingine ng’ombe anakimbia hovyo kama ana kichaa, na tatizo lilivyoanza tulipata vifo vya ghafla vya ng’ombe wawili katika mazizi tofauti, tulipowachunguza tuligundua mapafu yao yalikuwa yameharibika hivyo tukagundua kuwa ni ugonjwa wa mapafu,” alisema Dkt. Mbise

 

Aliongeza kuwa ugonjwa huo umekuwa ukisumbua sana katika eneo hilo ndio maana huwa wanachanja mifugo mara mbili kwa mwaka, kila baada ya miezi sita lakini kwa wakati huu ugonjwa umelipuka ghafla hivyo wameshaagiza chanjo kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa atayasimamia maagizo yote aliyoyatoa Waziri na kuhakikisha yanatekelezwa kama alivyoagiza huku akisema kuwa kufuatia maagizo hayo wameshaleta katika Ranchi hiyo dozi za chanjo 9500 kwa ajili ya kuchanja ng’ombe hao.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni