Nav bar

Jumatatu, 1 Julai 2019

SERIKALI YADHAMIRIA KUPUNGUZA UMASKINI KUPITIA ZAO LA NGOZI




Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imedhamiria kupunguza umasikini kwa kuboresha kipato cha wafanyabiashara na kuongeza ajira kwa wananchi kupitia zao la ngozi hususan ngozi itokanayo na wanyama wafugwao hapa nchini.

Hayo yamesemwa  na Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko, Dkt.Felix Nandonde wakati akifungua mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro mjini humo.

Dkt.Nandonde amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa washiriki wanaongeza utaalamu katika uchinjaji, uchunaji, ukaushaji, uhifadhi,usafirishaji na usindikaji ili kuzalisha ngozi bora itayokuwa na thamani zaidi.

Akiongelea mchango wa zao la ngozi kwenye pato la Taifa na la mtu mmoja, mmoja, Dkt.Nandonde alisema kuwa hadi mwezi Machi mwaka 2018/19 jumla ya sh.bil.5.2 zilikusanywa kutokana na usafirishaji ngozi na bidhaa zake nje ya nchi.

Akifafanua kuhusu sheria Na.18 ya Mwaka 2008, inayosimamia biashara ya ngozi nchini, Dkt.Nandonde alisema kuwa sheria hiyo inawataka wachunaji wote wa Ngozi kupata mafunzo na kupewa leseni za uchunaji ngozi.

Akihitimisha hotuba yake mgeni rasmi, Dkt.Nandonde alisema kuwa baada ya mafunzo hayo,Wizara ina mategemeo makubwa sana kuhusu mabadiliko ya ubora wa ngozi zinazozalishwa hapa nchini.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw.Gabriel Bura aliwataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo ya awali na kuahidi kuwa mafunzo mengine yataendelea kutolewa nchi nzima ikiwa ni kielelezo cha serikali kuitambua na kuithamini kada hiyo.

Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo wakiongea kwa nyakati tofauti wameishukuru sana serikali ya awamu ya tano kwa kuitambua na kuonyesha nia ya kuinua sekta hiyo kwa vitendo.

Aidha washiriki hao wameiomba serikali pia kuangalia uwezekano wa kuwatafutia masoko ya uhakika ili kuinua vipato vyao na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa.




Mgeni rasmi,Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko, Wizara ya  Mifugo na Uvuvi, Dkt.Felix Nandonde (kushoto) akiongea na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Bw.John Mgalula ofisini kwake leo kabla ya kufungua mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya manispaa hiyo.Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Msaidizi wa mazao ya mifugo, usalama wa chakula na lishe, Bw.Gabriel Bura.





Washiriki wa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro wakimsikiliza mgeni rasmi Dkt.Felix Nandonde (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja yanayofanyika mjini Morogoro  (12.6.2019).



Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt.Felix Nandonde (mwenye suti) kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya manispaa ya Morogoro mara baada ya ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo mjini Morogoro.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni