Nav bar

Jumatatu, 27 Mei 2019

TANZANIA YASHIRIKI KONGAMANO LA MATUMIZI ENDELEVU YA RASILIMALI ZA BAHARI NCHINI MSUMBIJI




Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi zikiwemo Tanzania, Kenya, Msumbiji na Afrika ya Kusini na Visiwa vya Ushelisheli zimepewa rai ya kuhakikisha zinafanya kila njia kulinda rasilimali za pamoja hususan zinazopakana na bahari ili ziweze kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizo.

Rai hiyo imetolewa na Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakati wa ufunguzi wa kongamano la kujadili matumizi endelevu ya rasilimali za bahari linaloendelea katika mji wa Maputo nchini humo.

Rais Nyusi amesema kongamano hilo la siku mbili lina umuhimu mkubwa kwa kuwa linafanyika wakati huu ambapo uvunaji holela na usiofuata utaratibu wa rasilimali za bahari umeshamiri katika nchi nyingi za bara la Afrika na Asia.

Akihutubia washiriki wa Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameelezea hatua mbalimbali ambazo nchi ya Tanzania imepiga katika kuhakikisha malengo ya milenia kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za asili yanafikiwa.

Mhe. Ulega amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kupambana na uvuvi haramu na biashara haramu ya utoroshwaji wa mazao ya uvuvi, kudhibiti uvuvi wa mabomu katika pwani ya Bahari ya Hindi, kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira ya bahari kwa lengo la kuinua maisha ya jamii za wavuvi, kulinda maeneo tengefu ya bahari, kufanya utafiti na kuzuia uharibifu wa bahari unaotokana na matumizi ya bidhaa za plastiki.

Aidha, Mhe. Ulega amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi kuhakikisha rasilimali zilizopo zinalindwa na zinazinufaisha nchi wanachama.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo umeangazia mchango wa sekta
zingine ambazo kwa pamoja zinachochea ukuaji wa uchumi wa bluu ambao
unahimiza matumizi ya bahari katika kukuza uchumi wa nchi.

Sekta hizo ni pamoja na usafirishaji, utalii wa bahari, uhifadhi wa mazingira, utafutaji na uchimbaji wa gesi, pamoja na usalama wa chakula na ajira.

Kwa pamoja washiriki wa kongamano hilo wamekubaliana katika kuimarisha ushirikiano, kuendelea kubadilishana uzoefu na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika ili kulinda rasilimali za bahari kwa kuwa baadhi ya rasilimali hizo hazina mipaka kama ilivyo kwa samaki aina ya jodari ambao huhama kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

Kongamano hilo limeandaliwa na nchi ya Msumbiji kwa kushirikiana na Norway pamoja na mashirika mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia, ambapo zaidi ya washiriki 300 kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwemo wataalam wa sayansi za bahari, mazingira, usafirishaji majini, viongozi wa kisiasa, wakuu wa mashirika ya fedha na mashirika binafsi yanayojihusisha na uhifadhi wa rasilimali za bahari wanahudhuria kongamano hilo.

Tanzania, imewakilishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na wengine ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Mmanga Mjengo Mjawiri, Mkurugenzi wa Uvuvi Zanzibar Mussa Aboud Jumbe na maofisa kutoka Mamlaka ya Bahari ya Kuu nchini.



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ( wa pili kutoka kulia) akifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye kongamano la matumizi endelevu ya rasilimali za bahari katika Mji wa Maputo, Nchini Msumbiji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega akihutubia washiriki kwenye kongamano la matumizi endelevu ya rasilimali za bahari lililofanyika katika mji wa Maputo, Nchini Msumbiji


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa katika mazungumzo na maafisa kutoka SMZ ambao pia wameshiriki kwenye kongamano la matumizi endelevu ya rasilimali za bahari katika mji wa Maputo  Nchini Msumbiji.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni