Nav bar

Jumatatu, 23 Oktoba 2017

WAZIRI MPINA NA WAZIRI WA OMAN WAZUNGUMZIA MASUALA YA UWEKEZAJI WA VIWANDA KATIKA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI

                                          NA MWANDISHI MAALUM
Waziri anayeshughlia masuala ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina amekutana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salim Al Ismail na kujadili suala zima la uwekezaji wa viwanda katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Katika Mazungumzo hayo Waziri Mpina amemueleza  Waziri huyo wa uwekezaji wa Oman kuwa Tanzania imekuwa ikizalisha nyama kwa kiasi cha tani 36 kwa siku na imekuwa ikifanya biashara kwa kuuza tani za nyama ambazo hazijakatwa katika nchi za falme za kiarabu ikiwemo Oman. 

Wakati umefika sasa kwa nchi hizi mbili kushirikiana kwa pamoja katika Sekta hii kwa Oman kuwekeza katika Viwanda vya ndani vya nyama kwa kuendeleza viwanda vilivyopo na hata kujenga Viwanda vipya, akitolea mfano ujenzi wa kiwanda cha nyama cha Ruvu ambao umefikia 51% kukamilika.

“Tunataka viwanda vyote vya nyama vya ndani vikidhi mahitaji na kuweza kuuza nyama nje ya nchi”. Alisema Mpina.

Kwa upande wake Waziri Salim Al Ismail alipoelezwa kuhusu viwango na madaraja mbali mbali ya nyama nchini na mmoja wa mtaalam kutoka wizara hiyo, alisema kuwa Oman ipo tayari kuwekeza katika sekta ya viwanda vya nyama na kuisaidia Tanzania kutafuta soko la Marekani kupitia Oman kwani nchi hiyo ya Falme za kiarabu ina cheti  na kibali kilichothibitishwa na mamlaka ya chakula na dawa cha Marekani.

 “Tunaweza kuchukua nyama kutoka Tanzania na kuingiza Marekani bila kulipa Ushuru, tunapaswa kuwa na vyeti halali ili kuweza kupata soko katika nchi nyingine, Alisema Waziri Ismail.”

Waziri Ismail aliendelea kusema kuwa, Makampuni Binafsi kutoka Oman yapo tayari kufanya biashara katika eneo hili hivyo ni wakati wa Tanzania sasa kuonyesha utayari.
“Hizi bidhaa za nyama ni lazima zitoke kwenu sababu sisi hatuna maji wala majani ya kulisha mifugo kama ngombe, mbuzi na kondoo ambao huchinjwa kwa wingi baada ya Hijja. Alisisitiza.”

Kwa Upande wa Sekta ya Uvuvi Waziri Huyo wa Oman alisema Oman imenunua teknolojia ya kisasa ya uwekezaji katika fukwe ya Bahari kutoka Texas Marekani, Teknolojia inayojulikana kitaalam kama Shrim farming inayoruhusu uzalishaji wa chakula cha samaki wavuliwao katika maji marefu bila kuharibu mazingira.

Alisema Tenkolijia hiyo inaweza kutumika katika uwekezaji wa Fukwe ya bahari ya Hindi akitolea mfano eneo la bagamoyo kwa kuzingatia tathmini ya athari ya mazingira na ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kuwasaidia wavuvi wadogo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  Dkt Yohana Budeba (Sekta ya Uvuvi) Alisema ni furaha yake kuona wafanya biashara wa Oman wanakuja kuwekeza Tanzania au kushirikiana na wavuvi wa ndani kwani kuna samaki wengi wa kutosha kumudu viwanda vya kuchakata  na kuwezesha biashara kubwa ya samaki.


Katika picha, wa pili kushoto Mhe. Luhaga Mpina Waziri wa Mifugo na Uvuvi akizungumzia masuala ya uwekezaji wa viwanda katika sekta ya mifugo wa pili kulia ni Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salim Al Ismail, akimsikiliza kwa makini. Kulia ni Balozi wa Oman nchini Mhe. Ali Mahroqi, na kushoto ni Katibu Mkuu  sekta ya Uvuvi Dkt. Yohana Budeba.


Kushoto Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salim Al Ismail, akimtembeza Mhe. Luhaga Mpina Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika meli ya Oman baada ya mazungumzo yaliyohusu sekta ya Mifugo na Uvuvi Dar es Salaam juzi.



 Katika Picha Majadiliano kati ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salim Al Ismail, na wataalam kutoka pande hizo mbili kuhusu uwekezaji kwenye sekta ya Mifugo na Uvuvi.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kulia akijadili jambo na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Mhe. Salim Al Ismail, baada ya kuuonyeshwa mandhali ya meli ya Oman iliyotia nanga katika bandari ya Dar es Salaam.


Wakiwa katika picha ya Pamoja ,Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Mhe. Luhaga Mpina, Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salim Al Ismail, Balozi wa Oman Nchini Mhe. Ali Mahroqi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) Dkt Yohana Budeba na watumishi wa Wizara hiyo baada ya Mawaziri hao kufanya mazungumzo kuhusiana na sekta ya Mifugo na Uvuvi juzi ndani ya meli ya Oman iliyotia nanga katika bandari ya Dar es salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni