Nav bar

Alhamisi, 19 Oktoba 2017

MAHAKAMA YATOA AMRI NG’OMBE WALIOTAIFISHWA KUPIGWA MNADA

                                     NA MWANDISHI MAALUM - MWANGA
NG’OMBE waliotaifishwa na serikali katika wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wanatarajiwa kupigwa mnada kufuatia uamuzi wa mahakama.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, wakati alipokwenda kukagua lindo la ng’ombe hao, jana eneo la Mgagao, wilayani Mwanga, walikohifadhiwa.

 “Kufuatia uamuzi wa mahakama, ng’ombe hawa watauzwa kwa njia ya mnada siku ya Ijumaa, Oktoba 20, mwaka huu, kutokana na hali za ng’ombe hawa kutokuwa nzuri”, alisema.

 Aliongeza, “Tayari mahakama imeridhia ombi la serikali la kutaka kuuzwa kwa ng’ombe hawa na ishamteua dalali wa kufanya mnada huo ambaye ni Marepelanto wa mjini Moshi na kazi hii itafanywa haraka kutokana na ng’ombe wengine kuanza kufa, kama mlivyosikia tayari sita wameshakufa”.

 Aidha alisema serikali itaanza operesheni maalum ya kuwakamata ng’ombe walioingizwa nchini kinyume cha sehria kuanzia Jumatatu ijayo.

 “Baada ya operesheni ya hapa Kilimanjaro, nilitoa siku saba kwa Mikoa mingine kuiondoa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume cha sheria kupitia Mikoa hiyo, muda huo umekwisha, Jumatatu tunaanza oparesheni nyingine itakayochukua siku 15 ili kuhakikisha mifugo hiyo inaondolewa yote”, alisema.

 Akijibu maswali kutoka kwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo, Bw. Mpina alisema kuwa iwapo kuna mifugo ya wenyeji ilikamatwa wakati wa operesheni hiyo wapeleke orodha ya ng’ombe hao kwa kupitia ngazi husika ili waweze kurudishiwa.

 “Wenyeji wenye ng’ombe waliokamatwa watumie taratibu zilizopo kwa kuanzia kwa viongozi wa maeneo wanayotoka hadi ngazi ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ikithibitishwa bila mashaka yoyote kuwa mifugo hiyo ni ya kwao zitatumika taratibu zinazohitajika kisheria kwa kuwa ng’ombe hawa sasa ni mali ya serikali”, alisema.

 Aidha alitoa onyo kwa viongozi hao kuhakikisha wanafanya zoezi hilo kwa weledi na kwamba iwapo watafanya udanganyifu hatua kali za kisheria zitachuliwa dhidi yao bila kujali nyadhifa zao.
 Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Maria Mashingo, aliyeiongoza operesheni hiyo, alisema kuwa mwendelezo wa operesheni hiyo imepelekea serikali kukamata ng’ome wengine takribani 2,000.
 “Tunawashukuru Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kutupatia ndege ambayo ilitusaidia sana katika zoezi hili tulilofanya kupitia vyombo vya ardhini na angani”, alisema.

 Alisema kuwa amebaini kuwa wizara ya Mifugo na Uvuvi ina changamoto ya uhitaji wa vifaa kama ndege kwani operesheni hiyo imebainisha wazi uhitaji huo.

 Awali akitoa rai yake kwa niaba ya wafugaji wenyeji ambao ng’ombe zao zimekamatwa kufuatia operesheni hiyo, Diwani wa Kata ya Kirya, Bw. Nyange Laizer aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa ng’ombe hizo kurudishiwa wenyewe.

 “Unajua sisi malisho yetu tunafanya hapa hapa na ndiyo maana operesheni hii ikawakumba na watu wetu na hii ni kutokana na ukweli kuwa huwezi kutofautisha ng’ombe za hapa kwetu na zile zinazoingizwa kinyume cha sheria”, alisema.

 Uamuzi huu wa mahakama unakuja baada ya ng’ombe hao kutaifishwa na serikali hivi karibuni baada ya kuingizwa hapa nchini kinyume cha sheria.


kulia Waziri Mpina akiongea kuhusu amri ya Mahakama ya kupigwa mnada ng'ombe 1325 waliotaifishwa na Serikali pembeni ni dalali aliyeteuliwa na Mahakama Bw.Mack Shayo wa kampuni ya MARIDELANTO ya Mjini Moshi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina katikati, kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Aaron Mbogho, kushoto kwake  katibu tawala wa wilaya ya Mwanga Bw. Yusuph  Kasuka wakiangalia ng'ombe waliotaifishwa  wakati wakinywa maji katika kijiji cha Mgagau wilayani Mwanga.


Ng’ombe walioamriwa na mahakama kupigwa mnada, mnada utafanyika siku ya ijumaa  Octoba 2017.Waziri Mpina katikati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Dkt. Maria Mashingo na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Aaron Mbogho wakijadili jambo baada ya kuongea na wanahabari kuhusu amri ya mahakama ya kupiga mnada ngombe walitaifishwa na Serikali.


Maoni 1 :